Akizungumza jana katika mkutano na waandishi wa habari akiwa pamoja na Rafael Grossi Mkurugenzi Mkuu wa Wakala wa Kimataifa wa Nishati ya Nyuklia (IAEA), Mohammad Eslami alisema: Pande mbili zina maelewano juu ya kuepuka lugha au vitendo ambavyo maadui wa Iran wanaweza kutumia.
Iran na Marekani, Jumamosi iliyopita zilianza mazungumzo huko Muscat mji mkuu wa Oman kuhusu miradi ya nyuklia ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran na kuhusu kuondoa vikwazo dhidi ya Jamhuri ya Kiislamu.
Pande mbili zimeyataja mazungumzo hayo kuwa yenye kuridhisha na zimekubaliana kuendelea na duru ya pili ya mazungumzo kesho Jumamosi.
Katika mkutano na waandishi wa habari, Eslami amesema mikutano ya ngazi ya manaibu kati ya wakala wa IAEA na Shirika la Nishati ya Atomiki la Iran itafanyika siku kadhaa zijazo ili kujadili masuala yaliyosalia na kuhusu ushirikiano wa pande mbili.
Mkuu wa Shirika la Nishati ya Atomiki la Iran amesisitiza kuwa taarifa ya pamoja ya mwaka 2023 kati ya Iran na IAEA imepelekea kupiga hatua chanya na kwamba masuala yaliyosalia yataendelea kupatiwa ufumbuzi kupitia mkondo huo huo.
Naye Rafael Grossi, Mkurugenzi Mkuu wa IAEA amesema wakala huo unawasiliana na maafisa wote wa Iran na wa Marekani ili kuwezesha kupiga hatua katika mazungumzo yao yasiyo ya moja kwa moja.
342/
Your Comment